
Msanii mkongwe wa muziki wa dancehall nchini Uganda, Bebe Cool, amepinga vikali madai yaliyoenezwa na Ziza Bafana kwamba alimkatia mawasiliano kwenye mitandao ya kijamii.
Kupitia taarifa aliyotoa kwenye vyombo vya habari na kurasa zake rasmi, Bebe Cool amesema hajawahi kumfungia msanii yeyote, akisisitiza kuwa madai hayo hayana msingi wowote.
“Siwezi kumfungia Ziza Bafana kwa sababu hana maarifa ya kutosha. Siwezi kumfungia msanii yeyote kwa sababu wana mengi ya kujifunza kutoka kwangu, ” alisema Bebe Cool.
Kauli hiyo inakuja baada ya Ziza Bafana kudai kuwa Bebe Cool alikata mawasiliano naye kwenye Instagram, Facebook, na mitandao mingine ya kijamii. Aidha, Ziza alidai kuwa hakulipwa stahiki zake baada ya kushiriki katika tamasha la Tondeka E Kiwatule, linaloandaliwa kila mwaka na Bebe Cool.
Hata hivyo, Bebe Cool amekanusha madai hayo na kusema hana sababu ya kukata mawasiliano na Ziza Bafana au msanii mwingine yeyote kwa sababu hana chuki binafsi na yeyote kwenye tasnia ya muziki. Ameongeza kuwa tofauti kati yao huenda zinatokana na kutoelewana au maneno ya mitaani yanayochochewa bila ushahidi wa moja kwa moja.
Hadi sasa, Ziza Bafana hajatoa majibu ya moja kwa moja kufuatia kauli hiyo mpya ya Bebe Cool, lakini mashabiki wameendelea kutoa maoni tofauti mitandaoni baadhi wakimtetea Bebe Cool na wengine wakimtaka Ziza kutoa ushahidi wa madai yake.