
Msanii maarufu kutoka Uganda, Jowy Landa, amevunja ukimya na kueleza hisia zake kuhusu kutokuwepo kwa baadhi ya wasanii katika mazishi ya kaka yake, aliyefariki wiki iliyopita kufuatia majeraha aliyopata baada ya kushambuliwa na wahalifu jijini Kampala.
Akizungumza kwenye mahojiano na kituo kimoja cha televisheni, Jowy alisema hakuwa na kinyongo na wale wasanii ambao hawakuhudhuria hafla hiyo, akieleza kuwa wengi wao walimfikia kwa njia binafsi kumpa pole.
“Ilikuwa ni msiba, siyo tamasha. Walioweza kufika walifika, lakini wengine walinitumia jumbe za rambirambi. Kama msanii A Pass, alinipigia simu kunifariji. Wasanii huwa na ratiba nyingi, kwa hiyo sioni kuwa ni jambo kubwa sana,” alieleza Jowy.
Aidha, alikanusha madai ya kuwepo kwa mgogoro baina yake na Nandor Love, akisisitiza kuwa bado ni marafiki wa karibu, japo kwa sasa kila mmoja anashughulika na majukumu tofauti.
“Sijawahi kuwa na bifu na Nandor Love. Tumekuwa marafiki wa karibu sana, ila kwa sasa kila mmoja ana shughuli zake. Mimi nipo na Team No Sleep (TNS), naye yupo Ghost Empire, hivyo hatupatani mara kwa mara kama zamani,” aliongeza.
Jowy Landa kwa sasa anaendelea na shughuli zake za muziki chini ya lebo ya TNS, huku akiendelea kupewa pole na mashabiki na wadau mbalimbali wa muziki kufuatia msiba huo mkubwa.