
Msanii wa muziki wa Dancehall nchini Uganda, Fik Gaza, amekanusha vikali madai kwamba alipokea fedha kutoka kwa watu wa karibu wa Rais Yoweri Kaguta Museveni (maarufu kama Sevo) kama kishawishi cha kujiunga na chama tawala cha National Resistance Movement (NRM).
Akizungumza katika mahojiano na kituo cha televisheni cha ndani, Fik Gaza alisema kuwa uamuzi wake wa kujiunga na NRM haukuhusiana na maslahi binafsi, bali ulikuwa wa kimkakati kwa ajili ya kuinua maisha ya watu wa mitaa ya walalahoi maarufu kama Ghetto.
Β βSikuvuka upande kwenda kwa Sevo kwa ajili ya pesa. Nilijiunga na NRM kumshukuru kwa msaada aliowahi kutoa kwa watu wa Ghetto, na kumuomba aendelee kusaidia β si kwa manufaa yangu binafsi kama inavyodaiwa,β alieleza Fik Gaza.
Tangu tangazo lake rasmi mapema mwezi huu katika hafla iliyofanyika Kampala na kuhudhuriwa na Rais Museveni, tetesi zilianza kusambaa kwamba msanii huyo alihongwa kwa βmagunia ya pesaβ ili kufanikisha uhamisho wake wa kisiasa. Lakini Fik Gaza amesisitiza kuwa ilikuwa ni uamuzi wa dhati unaolenga kuleta mabadiliko chanya kwa jamii yake.
Fik Gaza alikuwa mwanachama wa chama cha upinzani National Unity Platform (NUP), kinachoongozwa na msanii mwenzake Bobi Wine. Ingawa sasa yupo NRM, amesema bado anaheshimu na kudumisha urafiki na Bobi Wine, akisisitiza kuwa tofauti za kisiasa hazimaanishi uhasama wa binafsi.
Katika maelezo yake, Fik Gaza pia aliweka wazi kuwa amekuwa akishirikiana na serikali hata kabla ya kutangaza rasmi uamuzi wake, hasa kupitia Waziri wa Vijana Balaam Barugahare.
Akiwa mwanachama mpya wa NRM, Fik Gaza amesema yuko tayari kushirikiana na wasanii wengine wa chama hicho wakiwemo Alien Skin, Eddy Kenzo, Gravity Omutujju, na Bebe Cool, ili kueneza ujumbe wa Rais Museveni na kusaidia katika maendeleo ya vijana nchini.
Uamuzi huo umechochea mijadala mikubwa katika tasnia ya muziki na siasa za Uganda, huku baadhi wakimpongeza kwa kuchagua mwelekeo mpya wa kisiasa, na wengine wakimtuhumu kwa kusaliti harakati za vijana na wasanii wenzake