Gossip

Embarambamba Apiga Sarakasi Matopeni Akimshauri Matiang’i Aachane na Urais 2027

Embarambamba Apiga Sarakasi Matopeni Akimshauri Matiang’i Aachane na Urais 2027

Msanii kutoka Kisii anayefahamika kwa mbwembwe na utata wake jukwaani, Embarambamba, amerudi tena kwa kishindo mitandaoni kupitia wimbo mpya wa kisiasa unaomlenga moja kwa moja aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Kitaifa, Fred Matiang’i.

Kupitia video ya wimbo huo inayosambaa kwa kasi mitandaoni, Embarambamba ameibua mjadala mkubwa kwa kutumia mtindo wake wa kipekee wa kujigaragaza matopeni, kukimbia ovyo kama mtu aliyepagawa, na kurusha miguu hewani huku akitoa ujumbe mzito kisiasa kwa jazba ya aina yake.

Katika wimbo huo, Embarambamba anamsihi Matiang’i kuachana na ndoto ya kugombea urais mwaka 2027, akimshauri kushirikiana na Gavana wa Kisii, Simba Arati, waingie kwenye serikali ya Rais William Ruto ili kuwaletea wananchi maendeleo.

Video hiyo imeibua hisia mseto miongoni mwa Wakenya, huku baadhi wakieleza wasiwasi kuhusu afya ya akili ya msanii huyo, kutokana na jinsi anavyojihatarisha kimwili katika kila content yake. Wengine, hata hivyo, wamebaki wakicheka na kufurahia ubunifu wake wa kipekee, wakisema huenda ni njia ya kuvutia wasikilizaji kwa maudhui yenye uzito wa kisiasa.

Licha ya mjadala huo, hakuna anayeweza kutilia shaka kuwa Embarambamba amejenga jina lake kupitia utata, ucheshi, na ujasiri wa kusema mambo ambayo wengi huyaogopa, na wimbo huu mpya ni ushahidi mwingine wa namna anavyotumia sanaa kama silaha ya kuwasiliana moja kwa moja na jamii.