
Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) limeidhinisha ongezeko la idadi ya mashabiki watakaoruhusiwa kuhudhuria mechi ya robo fainali ya Kombe la Mataifa kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) kati ya Kenya na Madagascar itakayopigwa katika uwanja wa Kasarani. Idadi hiyo imeongezwa hadi asilimia 80 ya uwezo wa uwanja, baada ya ombi rasmi kutoka kwa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF).
Hatua hii inakuja baada ya CAF kupunguza idadi ya mashabiki hadi asilimia 60 wakati wa mechi ya mwisho ya Kundi A kati ya Kenya na Zambia. Uamuzi huo wa awali ulitokana na tukio la mashabiki kuingia uwanjani bila tiketi katika mechi iliyotangulia kati ya Kenya na Morocco. Hata hivyo, baada ya FKF kuchukua hatua za kudhibiti hali hiyo na kuimarisha usalama, CAF imekubali kuongeza idadi ya mashabiki, jambo linaloleta matumaini mapya kwa Harambee Stars kupata sapoti ya kutosha kutoka kwa mashabiki wao wa nyumbani.
Kenya itashuka dimbani leo jioni kuchuana na Madagascar katika mechi ya kwanza ya robo fainali, ikilenga kuendeleza mafanikio yake katika mashindano haya. Baadaye usiku huu, Tanzania itakutana na Morocco kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa.
Mashindano haya yanaendelea kuonyesha ushindani mkubwa miongoni mwa mataifa ya Afrika. Siku ya Jumamosi, Uganda itacheza dhidi ya Senegal kwenye uwanja wa Mandela, huku Sudan ikimenyana na Algeria katika mechi ya mwisho ya robo fainali itakayopigwa usiku huo katika uwanja wa Amani.
Mechi za nusu fainali zitafanyika Jumanne ijayo, na mshindi wa fainali atapatikana Jumamosi ijayo, siku moja baada ya mechi ya kutafuta mshindi wa tatu.