
Timu ya taifa ya Morocco (Atlas Lions) imeandika historia tena katika anga la soka barani Afrika baada ya kutwaa taji lake la tatu la Mashindano ya Soka kwa Wachezaji wa Ndani ya Afrika (CHAN), kwa kuichapa Madagascar kwa mabao 3-2 katika fainali ya kusisimua iliyopigwa katika Uwanja wa Kimataifa wa Kasarani, Nairobi.
Morocco, ambao waliwahi kutwaa taji hili mwaka 2018 na 2020, walionyesha kiwango cha juu licha ya upinzani mkali kutoka kwa Madagascar waliocheza kwa ari kubwa wakitafuta taji lao la kwanza.
Nyota wa mchezo huo alikuwa mshambulizi mahiri Oussama Lamlaoui, ambaye alitikisa nyavu mara mbili, ikiwa ni pamoja na bao maridadi alilofunga kutoka umbali wa yadi 40. Bao hilo la kipekee liliibua shangwe uwanjani na kumfanya kumaliza mashindano akiwa mfungaji bora kwa jumla ya mabao sita.
Ushindi huo haukuwa tu fahari kwa Morocco bali pia ulijumuisha zawadi nono ya pesa taslimu, shilingi milioni 453, ilhali washindi wa pili, Madagascar, waliyoonyesha kandanda safi, waliondoka na kitita cha shilingi milioni 155.
Fainali hiyo ya kuvutia ilihudhuriwa na viongozi wa juu wa soka na serikali, akiwemo Rais wa Kenya William Ruto, Rais wa Shirikisho la Soka Ulimwenguni (FIFA) Gianni Infantino, na Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) Patrice Motsepe. Uwepo wao uliongeza hadhi ya tukio hilo na kudhihirisha maendeleo ya soka barani Afrika.