
Serikali ya Kenya imeingia makubaliano na Shirikisho la Mpira wa Kikapu la Kitaifa (NBA) kujenga ukumbi wa kisasa wa kimataifa humu nchini. Uamuzi huu ulifikiwa katika mazungumzo kati ya Waziri wa Michezo, Salim Mvurya, na maafisa wakuu wa NBA wakiongozwa na Clare Akamanzi, afisa mkuu wa eneo la Bara Afrika.
Ukumbi huu utakaojengwa kwa kasi unatarajiwa kuwa na uwezo wa kuandaa mashindano ya mpira wa kikapu ya kimataifa, jambo litakalowawezesha wanamichezo wa Kenya kupata fursa kubwa zaidi za kuonyesha vipaji vyao na kushindana na wachezaji kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Serikali imeahidi kutoa eneo maalum kwa ajili ya ujenzi huo kama sehemu ya mikakati yake ya kukuza na kuendeleza talanta za michezo nchini.
Kwa upande wake, NBA itachangia kwa kiasi kikubwa katika fedha za ujenzi na itahakikisha ukumbi huo unakuwa mahali pa kisasa na lenye kuvutia, si tu kwa ajili ya michezo bali pia kwa ajili ya shughuli zingine za burudani. Mradi huu unatarajiwa pia kutoa ajira na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wanamichezo pamoja na jamii kwa ujumla.