Msanii wa muziki wa hip hop kutoka nchini Kenya, Khaligraph Jones, ameonyesha kutoridhishwa kwake na jinsi wasanii wanavyoshughulikiwa wakati wa matamasha na hafla mbalimbali, akisema kuwa wanapewa heshima kubwa wanapowasili lakini wanapuuzwa mara baada ya kufanya maonyesho yao.
Kupitia ujumbe aliouchapisha mitandaoni, Khaligraph amesema kuwa ni jambo la kusikitisha kuona wasanii wakiwasili kwenye matamasha wakiwa wamebebwa kwa magari ya kifahari, lakini baada ya kutumbuiza, wanalazimika kutumia magari ya huduma kama Uber kurejea majumbani mwao.
Papa Jones amesema hali hiyo inaonyesha ukosefu wa heshima na thamani kwa wasanii, licha ya mchango mkubwa wanaotoa katika burudani na kuinua tasnia ya muziki. Amesisitiza kuwa wasanii wanapaswa kuthaminiwa sawasawa na taaluma nyingine, kwani kazi yao pia inahusisha jasho, muda na ubunifu mkubwa.
Khaligraph ametoa wito kwa wadau wa muziki, waandaaji wa matamasha na serikali kutambua mchango wa wasanii na kuboresha namna wanavyohudumiwa ili kulinda heshima na hadhi ya tasnia ya muziki Afrika Mashariki.