Padre Michael Watenga amezua gumzo nchini Kenya baada ya kufanya ziara ya ghafla katika klabu maarufu ya burudani mjini Eldoret iitwayo Timba XO na kuwaacha wateja wakiwa na butwaa.
Kulingana na mashuhuda, padre huyo aliingia klabuni hapo akiwa mtulivu na mwenye tabasamu, kisha akaomba muziki uzimwe kwa muda mfupi.
Wateja, ambao awali walidhani ni tukio la kawaida la usalama au tangazo la dharura, walishangazwa kuona kwamba kiongozi huyo wa dini alikuwa amekuja kwa ibada maalum ya kuwabariki waliokuwepo.
Baada ya kuhubiri ujumbe mfupi kuhusu matumaini, upendo na umuhimu wa kutafuta njia sahihi maishani, Padre Watenga aliwaombea wale wote waliokuwa klabuni hapo na kukusanya sadaka, hatua iliyowashangaza zaidi waliokuwepo.
Baadhi ya wateja walichangia kwa hiari, wakisema kuwa hawajawahi kushuhudia jambo kama hilo katika klabu ya usiku.