Msanii wa Bongo Fleva Yammi amezua gumzo kubwa mitandaoni baada ya kudokeza uwezekano wa kolabo yake na staa wa kimataifa Diamond Platnumz.
Kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, Yammi ameposti picha ya pamoja na Diamond Platnumz, hatua iliyochochea hisia na mijadala miongoni mwa mashabiki wao. Kilichozidi kuwasha moto wa gumzo hilo ni ujumbe aliouambatanisha na picha hiyo akiwauliza mashabiki wake endapo angefanya wimbo na kaka yake Diamond Platnumz, wanadhani jina la wimbo huo lingekuwa lipi.
Ujumbe huo umewafanya mashabiki wengi kuamini kuwa kolabo hiyo iko njiani, huku wengine wakianza kupendekeza majina mbalimbali ya wimbo huo, wakieleza matumaini yao kuwa kazi hiyo itakuwa kubwa ndani na nje ya Afrika Mashariki.
Hata hivyo, hakuna uthibitisho rasmi kutoka kwa Yammi wala Diamond Platnumz kuhusu lini kolabo hiyo itafanyika au kama tayari imerekodiwa. Licha ya hilo, wengi wanaona kuwa endapo wawili hao wataungana, basi muziki wa Bongo Fleva utafaidika pakubwa kutokana na nguvu na ushawishi wao katika tasnia.