Mwimbaji wa muziki wa Injili, Jennifer Mugendi, amewataka wasanii kuwa waangalifu wanapoingia kwenye mikataba ya muziki, akisisitiza umuhimu wa kusoma kwa makini vipengele vyote vya mkataba kabla ya kuweka saini.
Akizungumza kuhusu uzoefu wake binafsi, Jennifer amesema kuwa aliwahi kudanganywa kwa maneno matamu na kuahidiwa mkataba wa miaka miwili, lakini baadaye aligundua kuwa alichosaini kilikuwa ni mkataba wa miaka kumi.
“Niliahidiwa kitu kimoja kwa maneno, lakini nilipoweka saini bila kusoma kwa makini, nikajikuta nimefungwa kwenye mkataba wa miaka kumi,” alisema Mugendi, akionya kuwa makosa kama hayo yanaweza kuwakwaza wasanii kimaendeleo na kifedha.
Mwimbaji huyo aliwataka wasanii, hasa wanaoanza safari yao ya muziki, kuhakikisha wanapata ushauri wa kisheria kabla ya kusaini mikataba yoyote, ili kuepuka kunaswa kwenye masharti magumu yanayoweza kudhoofisha vipaji vyao.
Ushauri wa Jennifer Mugendi umepokelewa vyema na wadau wa muziki, wengi wakisema ni funzo muhimu kwa wasanii chipukizi wanaotamani kufanikiwa bila kujikuta katika mitego ya mikataba isiyoeleweka.