Kampuni ya teknolojia ya Apple imetangaza kuwa itaanzisha chaguo jipya litakaloruhusu watumiaji kuchagua kiwango cha transparency katika muonekano wa mfumo mpya wa iPhone.
Hatua hii inakuja baada ya kuzinduliwa kwa design mpya inayojulikana kama Liquid Glass, ambayo inachanganya mwonekano wa kioo na maji, ikitoa hisia ya kisasa zaidi katika muundo wa iOS. Hata hivyo, Apple imekiri kuwa baadhi ya watumiaji, hasa wenye changamoto za kuona, wamekuwa wakipata ugumu kutofautisha icons na buttons kutokana na kiwango kikubwa cha uwazi katika muonekano huo.
Kupitia maboresho hayo, Apple imepanga kuweka sehemu maalum ya kuchagua kiwango cha uwazi (transparency level) kulingana na mapendeleo ya mtumiaji. Watumiaji wataweza kuchagua kati ya mitindo miwili ambazo ni Clear na Tinted.
Chaguo la Clear litaonyesha mandhari ya nyuma ya icons kwa uwazi zaidi, huku Tinted likiongeza opacity na contrast ili kufanya icons na buttons ziweze kuonekana kwa urahisi zaidi, hasa kwa watu wenye matatizo ya kuona.
Maboresho haya yanatarajiwa kujumuishwa katika toleo jipya la iOS litakalotolewa mwaka huu, hatua ambayo inalenga kuboresha matumizi na kupanua wigo wa upatikanaji kwa watumiaji wote.