Mashabiki Wazua Gumzo Kuhusu Ujauzito wa Mke wa Stevo Simple Boy

Mashabiki Wazua Gumzo Kuhusu Ujauzito wa Mke wa Stevo Simple Boy

Wajuzi wa mambo na mashabiki mtandaoni wameibua gumzo kubwa wakitilia shaka ujauzito wa mke wa msanii Stevo Simple Boy, wakidai kuwa ameonekana kuwa mjamzito kwa muda mrefu zaidi ya kawaida. Kwenye mijadala mitandaoni, baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wamedai kuwa ujauzito huo huenda unatumika kama kiki ya kumtangaza Stevo kwenye mitandao badala ya hali halisi ya uzazi. Wengine wameenda mbali zaidi wakitaka uongozi wa msanii huyo kumtafutia Stevo mke halisi, wakihisi kuwa anatumika vibaya kwa masuala ya kujitafutia umaarufu. Baadhi ya mashabiki wamesema kuwa hali hiyo inamkosea heshima Stevo Simple Boy, ambaye mara kwa mara amekuwa akijulikana kwa unyenyekevu na maisha ya kawaida. Wamesema kuwa msanii huyo anapaswa kulindwa dhidi ya watu wanaotumia jina lake kwa maslahi binafsi. Licha ya tetesi hizo kusambaa, Stevo Simple Boy na mkewe hawajatoa kauli rasmi kuhusu madai hayo, huku mashabiki wakingoja ufafanuzi zaidi.

Read More
 Khaligraph Jones Adokeza Kolabo Mpya na Msanii Chipukizi Toxic Lyrikali

Khaligraph Jones Adokeza Kolabo Mpya na Msanii Chipukizi Toxic Lyrikali

Mfalme wa rap nchini Kenya, Khaligraph Jones, amedokeza uwezekano wa kufanya kolabo na msanii anayechipukia kwa kasi, Toxic Lyrikali, huku akimsifia kwa kuendelea kushikilia mizizi ya rap nchini humo. Kupitia mazungumzo yaliyowekwa wazi na mdau wa muziki Thithad3, Khaligraph ameonyesha kuvutiwa na kazi ya Toxic, akisema kuwa kwa sasa ndiye anayeshikilia uhalisia wa rap nchini humo. Ameongeza kuwa iwapo watashirikiana kwenye wimbo, itakuwa ni kwa muda muafaka bila presha wala haraka. Iwapo kolabo hiyo itatimia, itakuwa moja ya ushirikiano unaosubiriwa kwa hamu zaidi katika muziki wa hip hop wa Kenya mwaka huu. Toxic Lyrikali, ambaye amekuwa akipata umaarufu kutokana na mtindo wake wa uandishi wa mashairi makali na uhalisia wa mitaani, anaendelea kutajwa kama mmoja wa wasanii wanaochukua nafasi kubwa katika kizazi kipya cha muziki wa hip hop nchini Kenya.

Read More
 Mahakama Yakataa Kuondoa Video ya Utata ya Robert Burale

Mahakama Yakataa Kuondoa Video ya Utata ya Robert Burale

Mhubiri mwenye utata nchini Kenya Robert Burale amepata pigo kubwa baada ya mahakama ya Nairobi kukataa ombi lake la kutaka mahojiano ya video yaliyofanywa na mke wake wa zamani, Rozina Mwakideu, yafutwe na kuondolewa kwenye mitandao ya kijamii. Katika uamuzi uliotolewa Jumanne,Mahakama imekataa ombi hilo la kuondoa video hiyo mtandaoni, lakini ikaamuru Rozina na Alex Mwakideu kuacha kuchapisha au kusambaza tena mahojiano hayo yenye utata. Hakimu mkaazi wa mahakama ya Milimani, Thomas Nzyoki, amesema kuwa amri iliyotolewa ni ya muda na inalenga kuzuia uchapishaji wowote mpya wa video hiyo kwenye mitandao ya kijamii hadi kesi itakaposikilizwa na kuamuliwa. Amefafanua pia kuwa hatua hiyo haiathiri video ambayo tayari ipo mtandaoni. Wakili anayewakilisha Rozina na Alex Mwakideu, Ochiel Dudley, ameiambia mahakama kuwa wateja wake wataheshimu kikamilifu maagizo yaliyotolewa. Kesi hiyo itatajwa tena tarehe 25 Februari 2026 ili kuhakikisha kuwa pande zote zimewasilisha hoja zao za maandishi. Pasta Burale aliwashtaki Rozina na Alex akiwatuhumu kwa kumdhalilisha (defamation) na kudai fidia ya shilingi milioni 20 za Kenya, akitaka pia mahakama iamuru video hiyo iondolewe mtandaoni na washtakiwa kuomba msamaha hadharani.

Read More
 Diamond Platnumz Awatolea Uvivu Waliodai Hana Elimu

Diamond Platnumz Awatolea Uvivu Waliodai Hana Elimu

Staa wa muziki kutoka Tanzania, Diamond Platnumz, amewatolea uvivu wasomi waliowahi kudai kuwa hana kisomo, akisema elimu ya mtaa imemfungulia milango mingi zaidi ya wale wenye madigrii. Akizungumza kwenye hafla ya siasa, amesema kuwa wakati anaanza safari yake ya muziki, alikumbana na dhihaka na kejeli kutoka kwa watu waliomwona kama asiye na elimu ya kutosha, jambo lililomkatisha tamaa kwa muda. Hata hivyo, anasema aliamua kutumia ujuzi wa mtaani na nidhamu ya kazi kufikia mafanikio makubwa ambayo sasa yanamtambulisha kimataifa. Msanii huyo, amefafanua kuwa licha ya kupitia changamoto nyingi awali, kwa sasa ndiye msanii anayebeba bendera ya Tanzania kimataifa, akionesha kwamba elimu rasmi si kigezo pekee cha mafanikio. Diamond pia amegusia kazi zake tatu mpya alizoziachia mwezi huu wa Oktoba, “Msumari,” “Nani,” na “Sasampa”, akieleza kuwa amezitoa kwa makusudi ili kuwakemea waliodai amepoteza umaarufu wake. Hata hivyo amesema nyimbo hizo ni uthibitisho kwamba bado ana nguvu kubwa kwenye tasnia ya muziki, na kwamba elimu ya mtaa imemwezesha kufanikisha ndoto ambazo wengi wenye madigrii bado wanazisubiri.

Read More
 Zari Hassan Awaonya Wanawake dhidi ya Kuzaa Bila Uhakika wa Kifedha

Zari Hassan Awaonya Wanawake dhidi ya Kuzaa Bila Uhakika wa Kifedha

Socialite mwenye asili ya Uganda, Zari Hassan, ametoa onyo kali kwa wanawake kuhusu kupata watoto bila maandalizi ya kifedha. Zari anasema katika dunia ya sasa, upendo pekee hauwezi kuendesha familia, akisisitiza kwamba wanawake wanapaswa kuwa na uhuru wa kifedha ili kuishi na kulea watoto bila kutegemea wanaume. Mwanamama huyo wa watoto watano, ameeleza kuwa ni muhimu kwa mwanamke kujijengea msingi imara wa kiuchumi kabla ya kuingia kwenye majukumu ya uzazi, kwani mahusiano yanaweza kubadilika ghafla. Kwa mujibu wa Zari, mahusiano yanayojengwa tu kwa mapenzi au mvuto wa kimwili mara nyingi hayadumu, na mwisho wa siku wanawake wengi huishia kulea watoto wao pekee. Hata hivyo amesema kuwa mwanamke ambaye hana uwezo wa kifedha hana sababu ya kupata mtoto hadi atakapokuwa imara kiuchumi.

Read More
 Vera Sidika Afichua Kununua iPhone zake Kutoka Maduka Rasmi Marekani

Vera Sidika Afichua Kununua iPhone zake Kutoka Maduka Rasmi Marekani

Socialite kutoka Kenya, Vera Sidika, amefichua kuwa hununua simu zake za iPhone moja kwa moja kutoka maduka rasmi ya Apple nchini Marekani na siyo Kenya kama namna baadhi ya watu wanavyodai. Kupitia mitandao yake ya kijamii, Vera amesema kuwa hana imani na maduka mengi yanayouza vifaa vya teknolojia nchini humo, akieleza kuwa baadhi ya simu hizo huwa hazitoki moja kwa moja kwa Apple na huwa zimefanyiwa marekebisho kabla ya kuuzwa. Mama huyo wa watoto wawili, amesema hatua hiyo ni njia yake ya kujihakikishia ubora na usalama wa kifaa anachonunua, ikizingatiwa kwamba bidhaa ghushi zimekuwa changamoto kubwa sokoni. Kauli yake imezua mjadala mtandaoni, huku baadhi ya mashabiki wakimuunga mkono kwa kusema kuwa bidhaa bandia zimekuwa changamoto kubwa sokoni, huku wengine wakidai kuwa anajaribu kuonesha maisha ya kifahari.

Read More
 Oga Obinna Atokwa na Machozi kwenye Mazishi ya Kimani Mbugua

Oga Obinna Atokwa na Machozi kwenye Mazishi ya Kimani Mbugua

Mtangazaji Oga Obinna amejipata akitokwa na machozi ya uchungu wakati wa mazishi ya mwanahabari Kimani Mbugua, tukio lililofanyika katika eneo la Maragua, Kaunti ya Murang’a. Katika hotuba yake, Obinna ameelezea maumivu makubwa aliyoyahisi kutokana na kumpoteza rafiki katika tasnia ya habari, akisema wanahabari na wasanii wengi wanapitia changamoto kubwa za kimaisha na kisaikolojia ambazo mara nyingi hawawezi kuzungumzia hadharani. Ameeleza kuwa tasnia ya habari na burudani imejaa mashindano, presha na upweke unaowafanya wengi kukosa msaada wa kihisia. Amehimiza mastaa kusaidiana na kuinua kila mmoja badala ya kuendeleza mashindano na chuki zisizo na maana. Obinna pia amewakumbusha mashabiki kwamba maisha halisi ni tofauti kabisa na yanayoonekana kwenye mitandao ya kijamii, akibainisha kuwa mitandao hiyo mara nyingi huficha maumivu na mapambano ambayo watu hupitia kimya kimya. Mazishi ya Kimani Mbugua, aliyewahi kuwa mtangazaji mwenye kipaji kikubwa, yalihudhuriwa na watu wengi kutoka sekta ya habari na burudani nchini. Wengi walimkumbuka kama kijana mwenye ndoto kubwa, ubunifu na moyo wa kujituma.

Read More
 Mara Sugar Yatoka Sare ya Mabao 2–2 na Sofapaka FC Katika Ligi Kuu ya FKF

Mara Sugar Yatoka Sare ya Mabao 2–2 na Sofapaka FC Katika Ligi Kuu ya FKF

Timu ya Sofapaka FC imeonyesha ari kubwa ya kupambana baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Mara Sugar katika mechi ya Ligi Kuu ya FKF iliyochezwa kwenye uwanja wa Dandora. Mara Sugar ilianza kwa nguvu kipindi cha pili na kufanikiwa kupata bao la kwanza dakika ya 57, kabla ya kuongeza la pili dakika ya 68, na kuonekana kuwa njiani kuchukua alama tatu muhimu. Hata hivyo, Sofapaka haikukata tamaa. Timu hiyo ilirudi mchezoni kwa bao la kwanza dakika ya 72, na kuendelea kushambulia kwa nguvu hadi kufanikiwa kusawazisha dakika ya 95, na hivyo kunyakua alama moja muhimu. Kufuatia matokeo hayo, Mara Sugar sasa inashikilia nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na alama 6, huku Sofapaka ikishika nafasi ya 13 ikiwa na alama 5. Ligi hiyo itaendelea leo kwa mechi kadhaa zenye ushindani mkali ambapo Tusker itachuana na Kariobangi Sharks, Ulinzi Stars itavaana na Bidco United, Shabana itaikaribisha AFC Leopards, huku Kakamega Homeboyz wakipambana na APS Bomet.

Read More
 Apple Yasogeza Uzinduzi wa iPhone 18 Hadi Mwaka 2027

Apple Yasogeza Uzinduzi wa iPhone 18 Hadi Mwaka 2027

Kampuni ya teknolojia ya Apple imetangaza kuwa haitatoa toleo jipya la iPhone 18 mwaka 2026 kama ilivyokuwa ikitarajiwa, bali uzinduzi huo utafanyika mapema mwaka 2027. Kupitia taarifa rasmi, Apple imeeleza kuwa uamuzi huo umechochewa na dhamira ya kutoa muda zaidi kwa timu zake za maendeleo kuboresha teknolojia mpya itakayofanya iPhone 18 kuwa tofauti kabisa na matoleo yaliyotangulia. Kwa mujibu wa kampuni hiyo, mabadiliko hayo yanahusisha ubunifu mkubwa katika muundo, kamera, na teknolojia ya akili bandia (AI) ambayo inatarajiwa kuwa sehemu kuu ya mfumo wa iOS mpya. Taarifa hiyo imeibua hisia mseto miongoni mwa mashabiki wa Apple duniani, wengi wakionyesha hamu ya kujua ni mageuzi gani makubwa kampuni hiyo inapanga kuleta baada ya kuchukua muda wa ziada. Kwa sasa, Apple inaendelea na mauzo ya iPhone 17, huku ikiahidi kuwa iPhone 18 itakuwa hatua kubwa ya kihistoria katika mageuzi ya simu janja.

Read More
 Bahati Asema Mashabiki Wanatamani Maisha Yake na Diana Marua

Bahati Asema Mashabiki Wanatamani Maisha Yake na Diana Marua

Mwanamuziki mwenye utata nchini Kenya, Bahati, ameibua mjadala mtandaoni baada ya kudai kuwa mashabiki wake wanatamani maisha anayoyaishi na mke wake, Diana Marua. Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Bahati amepakia video akiwa na mkewe Diana wakifurahia mvinyo (wine) huku wakipigana mabusu hadharani licha ya maneno ya watu. Katika video hiyo mpya, Bahati amesema kuwa alikuwa anasoma maoni ya mashabiki kuhusu ukosoaji wa video yake ya awali, akisisitiza kuwa wengi wanatamani maisha yao ya kifahari na kimahaba. Kauli yake imejiri saa chache baada ya mwanamuziki huyo kukosolewa vikali mitandaoni kwa kuchapisha video nyingine akiwa amevaa chupi, hatua iliyozua mjadala mkubwa kuhusu mienendo yake ya kisanii na maisha binafsi.

Read More
 Juventus Yamtimua Kocha Igor Tudor Baada ya Msururu wa Vipigo

Juventus Yamtimua Kocha Igor Tudor Baada ya Msururu wa Vipigo

Miamba wa soka nchini Italia, Juventus, wametangaza kumfuta kazi kocha wao Igor Tudor kufuatia msururu wa matokeo duni uliomalizika kwa kichapo cha 3-0 dhidi ya Lazio Jumapili iliyopita. Kocha huyo raia wa Croatia, mwenye umri wa miaka 43, alijiunga na Juventus mwezi Machi kuchukua nafasi ya Thiago Motta, lakini ameshindwa kuipa timu matokeo chanya. Tangu achukue usukani, Juventus imepoteza mechi nane mfululizo, hali iliyowaacha katika nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi ya Serie A. Kichapo dhidi ya Lazio kilikuwa cha tatu mfululizo kwa timu hiyo katika mashindano yote, na kimechochea uamuzi wa uongozi wa klabu kumtimua kocha huyo. Kupitia taarifa rasmi, Juventus imetangaza kuwa Massimiliano Brambilla atachukua majukumu ya muda na kuiongoza timu kwenye mechi ijayo ya Serie A dhidi ya Udinese. Kwa sasa, Juventus wana alama sita nyuma ya vinara Napoli, wakiwa wamepoteza mechi tano zilizopita za ligi. Aidha, katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, klabu hiyo inashikilia nafasi ya 25 kwenye msimamo wa makundi baada ya kupoteza mechi moja na kutoka sare mara mbili katika mechi tatu za mwanzo. Hatua hii inaonekana kama jaribio la kuokoa msimu wa Juventus ambao umetikiswa na matokeo mabaya na ukosefu wa uthabiti tangu mwanzo wa mwaka huu.

Read More
 WhatsApp Yaanza Majaribio ya Kutaja Wajumbe Wote wa Kundi kwa Pamoja

WhatsApp Yaanza Majaribio ya Kutaja Wajumbe Wote wa Kundi kwa Pamoja

Kampuni ya WhatsApp imeanza kufanya majaribio ya kipengele kipya kinachowawezesha watumiaji kutaja wajumbe wote wa kundi kwa mara moja, badala ya kutumia alama ya @ kwa kila jina mmoja baada ya jingine. Kupitia kipengele hicho, kila mshiriki wa kundi atapokea taarifa (notification) inayoonyesha kuwa ametajwa kwenye ujumbe fulani. Hatua hii inalenga kuongeza ufanisi wa mawasiliano hasa kwenye makundi ya kazi, familia, na miradi ya kikazi ambapo ujumbe muhimu unahitaji kuwafikia watu wote kwa haraka. Kipengele hicho kipya kinatarajiwa kusaidia sana watumiaji wanaoshirikiana kwenye miradi au mijadala mikubwa, kwani kitapunguza muda wa kuandika na kuhakikisha kila mshiriki anapokea ujumbe muhimu. Wataalamu wa masuala ya teknolojia wanasema kuwa hatua hii ni ishara kwamba WhatsApp inaendelea kuimarisha huduma zake kuelekea mfumo wa community-style interaction, sawa na ule unaotumika kwenye majukwaa kama Telegram na Discord. Kwa sasa, kipengele hicho kipo katika hatua za majaribio, na kitarajiwa kuzinduliwa rasmi baada ya majaribio kukamilika na kupata mrejesho mzuri kutoka kwa watumiaji.

Read More