
Baraza la Sanaa la Tanzania (BASATA) limetoa siku mbili juu ya Sakata la msanii wa bongo fleva Harmonize na wasanii Killy na Cheed, kuweka sawa yote waliyokubaliana katika mkataba kama walivyoandikishana.
Hayo yamebainishwa na Afisa sanaa mwandamizi wa BASATA, Abel Ndaga katika kikao cha pili kilichopangwa kukutanisha pande zote mbili baada ya kikao cha kwanza kilichopangwa Oktoba 12, 2022 ambapo vikao vyote msanii Harmonize hakuweza kuhudhuria.
“Tumejadiliana vizuri kwenye kikao na kila kitu kimeenda sawa. Tumewapa siku mbili waweke mambo sawa na kurudi hapa kwa kuwa kila kitu kwenye mkataba kinajieleza.” amesema Abel Ndaga.
Hata hivyo BASATA imesema katika kikao kinachofuata lazima Harmonize mwenyewe awepo na hawatohitaji kumuona mwakilishi kwa kuwa uamuzi unakwenda kutolewa rasmi. Menejimenti ya Konde Music Worldwide ilitangaza kuachana na Wanamuziki hao Oktoba 4 mwaka huu.