Msanii aliyegeukia siasa, Bobi Wine, amesema hatouacha muziki hata kama atachaguliwa kuwa rais ajaye wa Uganda.
Kiongozi huyo wa chama cha NUP amesema muziki ni sehemu ya maisha yake na utambulisho wake, na hakuna kitu kinachoweza kumtenganisha nao hata madaraka ya juu kabisa ya nchi.
Akizungumza na wanahabari, Bobi Wine amesema kuwa muziki wake umekuwa sauti ya wananchi, hasa vijana na watu wa tabaka la chini, na ameapa kuendelea kuutumia kama chombo cha kuhamasisha, kuelimisha na kuunganisha Wauganda.
Mgombea huyo wa urais ambaye anapambana na Rais wa sasa Yoweri Kaguta Museveni wa chama cha NRM, ameonyesha imani kubwa ya kupata uungwaji mkono mkubwa kutoka maeneo mbalimbali nchini humo huku Uganda ikielekea kwenye wiki yenye mvutano mkubwa wa kisiasa.
Waganda wanatarajiwa kupiga kura Alhamisi hii, ambapo uchaguzi wa urais utakuwa kivutio kikuu ikizingatiwa kuwa Bobi Wine na Museveni watachuana vikali kwenye kinyang’anyiro hicho.