Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) limethibitisha kuwa litaanza kutumia teknolojia ya Video Assistant Referee (VAR) katika mechi za mchujo za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2026 zitakazochezwa baadaye mwezi huu.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi, teknolojia hiyo itatumika kwa mara ya kwanza kwenye mechi za nusu fainali zitakazochezwa tarehe 13 mwezi huu, ambapo Nigeria itamenyana na Gabon, huku Cameroon ikipambana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DR Congo) katika pambano jingine la siku hiyo hiyo.
Washindi wa michezo hiyo miwili watakutana kwenye fainali kuwania tiketi ya mwisho ya Afrika kuelekea fainali za Kombe la Dunia 2026.
Uamuzi wa CAF kuanzisha VAR katika hatua hii unaonekana kama hatua kubwa ya mageuzi katika usimamizi wa mechi muhimu za bara hilo. Awali, teknolojia hiyo haikutumika katika baadhi ya mechi kuu za mchujo, hali iliyosababisha malalamiko na maamuzi yenye utata kutoka kwa wadau wa soka.
Kwa mujibu wa CAF, teknolojia hiyo itawezesha kila tukio muhimu ikiwa ni pamoja na mabao, penalti, na kadi nyekundu kuchunguzwa kwa umakini zaidi ili kuhakikisha haki inatendeka uwanjani.
Wachambuzi wa soka wanasema hatua hii ni mwanzo wa enzi mpya ya uwazi na usawa katika soka la Afrika, huku mashabiki wakisubiri kuona jinsi VAR itakavyoathiri matokeo ya mechi hizi muhimu za kufuzu.