Msanii nyota wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz, amejitokeza kukanusha madai yaliyosambaa mtandaoni kwamba amekimbilia Dubai kufuatia machafuko yaliyoshuhudiwa nchini Tanzania baada ya uchaguzi wa Oktoba 29.
Tetesi hizo zilidai kuwa Diamond na familia yake waliondoka nchini Tanzania kwa hofu ya kushambuliwa, baada ya baadhi ya biashara za wasanii waliomuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kuripotiwa kushambuliwa na waandamanaji waliopinga uchaguzi huo.
Aidha, uvumi mwingine uliozua gumzo ulidai kuwa Wakenya walimpa makataa ya saa sita kuondoka kwenye hoteli moja eneo la Nyali, Kaunti ya Mombasa, baada kudaiwa kukimbilia Kenya . Hata hivyo, Diamond alijibu kupitia ukurasa wake mmoja wa udaku nchini Kenya kwa kuandika “Media 😅”, akionekana kushangazwa na taarifa hizo ambazo alizitaja kama uvumi wa mitandaoni.
Baada ya tukio hilo, Diamond amerejesha picha ya Rais Samia Suluhu Hassan kwenye ukurasa wake wa Instagram, muda mfupi baada ya kiongozi huyo kuapishwa rasmi kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hii inakuja siku chache baada ya msanii huyo kufuta picha na video zote zilizomuonyesha akimpigia kampeni kabla ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29.