 
									Staa wa muziki kutoka Tanzania, Diamond Platnumz, amewatolea uvivu wasomi waliowahi kudai kuwa hana kisomo, akisema elimu ya mtaa imemfungulia milango mingi zaidi ya wale wenye madigrii.
Akizungumza kwenye hafla ya siasa, amesema kuwa wakati anaanza safari yake ya muziki, alikumbana na dhihaka na kejeli kutoka kwa watu waliomwona kama asiye na elimu ya kutosha, jambo lililomkatisha tamaa kwa muda. Hata hivyo, anasema aliamua kutumia ujuzi wa mtaani na nidhamu ya kazi kufikia mafanikio makubwa ambayo sasa yanamtambulisha kimataifa.
Msanii huyo, amefafanua kuwa licha ya kupitia changamoto nyingi awali, kwa sasa ndiye msanii anayebeba bendera ya Tanzania kimataifa, akionesha kwamba elimu rasmi si kigezo pekee cha mafanikio.
Diamond pia amegusia kazi zake tatu mpya alizoziachia mwezi huu wa Oktoba, “Msumari,” “Nani,” na “Sasampa”, akieleza kuwa amezitoa kwa makusudi ili kuwakemea waliodai amepoteza umaarufu wake.
Hata hivyo amesema nyimbo hizo ni uthibitisho kwamba bado ana nguvu kubwa kwenye tasnia ya muziki, na kwamba elimu ya mtaa imemwezesha kufanikisha ndoto ambazo wengi wenye madigrii bado wanazisubiri.
 
								 
             
             
                             
                             
                             
                             
                             
                             
                            