Msanii nyota wa Uganda Eddy Kenzo ameomba radhi kwa fanilia na mashabiki wa Bebe Cool baada ya kuzua gumzo mitandaoni kufuatia maneno mazito ya matusi aliyotoa dhidi ya msanii huyo hadharani.
Akizungumza kituo kimoja cha habari nchini Uganda, Eddy Kenzo amesema kuwa hasira na maumivu ya kihisia vilimpelekea kutumia lugha isiyofaa mbele ya umma. Amesema kuwa hakukusudia kuwavunjia heshima mashabiki wa Bebe Cool wala kuharibu mshikamano wa wasanii.
Hitmaker huyo wa Nsimbudde, amekiri hadharani hatarudia tena kitendo hicho ambacho amedai kimemshushia hadhi kama rais wa shirikisho la wasanii Uganda na mshauri wa raisi kwenye masuala ya sanaa. Amesisitiza kuwa tofauti za kimtazamo kuhusu muziki zinapaswa kujadiliwa kwa heshima na si kwa maneno makali.
Sakata la wasanii hao wawili lilianza baada ya Bebe Cool kushindwa kuujumuisha wimbo wa “Nkulowozako” wa Eddy Kenzo kwenye orodha yake ya nyimbo kali za mwaka 2025, orodha ambayo huichapisha kila mwaka kama tathmini ya muziki wa Uganda. Hatua hiyo ilimkera Kenzo na kumfanya kutoa maneno mazito yaliyotafsiriwa na wengi kama matusi yasiyokuwa na staha.