Sports news

Eliud Kipchoge Kukutana Tena na Kenenisa Bekele Kwenye Marathoni ya New York

Eliud Kipchoge Kukutana Tena na Kenenisa Bekele Kwenye Marathoni ya New York

Mwanariadha mashuhuri wa Kenya, Eliud Kipchoge, anatarajiwa kukutana tena na mpinzani wake wa muda mrefu Kenenisa Bekele kutoka Ethiopia kwenye mbio za Marathoni za Jijini New York zitakazofanyika tarehe 2 Novemba mwaka huu.

Bekele, ambaye ni mmoja wa wanariadha bora wa mbio za masafa marefu katika historia, amejumuishwa kwenye orodha ya washiriki akichukua nafasi ya bingwa wa mwaka 2022, Evans Chebet.

Kipchoge na Bekele wamewahi kukutana mara tano kwenye mbio za marathoni, na safari hii inatarajiwa kuwasha upya ushindani mkali kati yao. Kwa upande wa Kipchoge, hii itakuwa mara yake ya kwanza kushiriki katika marathoni ya New York, huku Bekele akirejea baada ya mbio zake za mwisho mwaka 2021, ambapo alimaliza katika nafasi ya sita.

Katika michezo ya Olimpiki ya Paris mwaka 2024, Bekele alimaliza wa 39 kwa muda wa saa mbili dakika kumi na mbili na sekunde ishirini na nne, ilihali Kipchoge hakuweza kumaliza kutokana na jeraha la nyonga.

Mashindano haya yanatarajiwa kuvutia macho ya mashabiki wa riadha duniani kote, huku wawili hao wakipimana ubabe kwenye jiji la New York.

Kwa Eliud Kipchoge, mbio hizi ni sehemu ya azma yake ya kushiriki mbio zote saba kuu za Abbott World Marathon Majors.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *