
Mwanamitindo wa kimataifa kutoka nchini Tanzania Flaviana Matata ametoa rai kwa watu kutowadhihaki wanawake wanaopewa talaka kwani ni mengi wanayapitia mpaka kufikia uamuzi huo.
Flaviana ameeleza hayo kwa kupitia mfano wa mwanamuziki Adele ambaye amefanya mahojiano hivi karibuni na Oprah na kufunguka kuhusu kutalakiwa kwake.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram Flaviana amesema kuwa ifike muda jamii isiwadhihaki wanawake wanaopewa talaka. Mrembo huyo ameenda mbali zaidi na kusema kwamba mwaka wa 2019 baada ya kuachana na mume wake alisimangwa sana na kudhihakiwa na watu kwenye mitandao ya kijamii kama aliuwa mtu.
Flaviana anasema ni wanawake wachache ambao wanaweza kuweka wazi magumu wanayopitia kwenye ndoa zao kwani hakuna mwanamke anayependa kufunga ndoa na kuachika ila hutokana na sababu za msingi mpaka talaka kutolewa. Matata amehitimisha kwa kuisihi jamii kuacha kuwalaumu wanawake pale ndoa zao zinapovunjika.