Msanii wa Bongo Flava Harmonize ameweka wazi kuwa amemalizana rasmi na aliyekuwa mke wake raia wa Italia, Sarah, baada ya kumlipa kiasi cha euro elfu hamsini (€50,000) ili kumaliza mgogoro wao uliokuwa umefikishwa mahakamani.
Kupitia video aliyochapisha mtandaoni, Harmonize amesema kuwa licha ya changamoto zilizowahi kutokea kati yao, Sarah alikuwa na mchango mkubwa katika maisha na mafanikio yake. Kutokana na hilo, ameamua kukaa chini na familia ya aliyekuwa mke wake huyo ili kufikia makubaliano ya kumaliza tofauti zao kwa amani.
Msanii huyo ameeleza kuwa walikubaliana kuhusu kiasi cha fedha kilichotajwa na tayari amekilipa ili kufunga kabisa suala hilo lililokuwa limefika mahakamani. Aidha, amesema alimshirikisha pia mpenzi wake wa sasa, Kajala Masanja, katika maamuzi hayo ili kuwe na uwazi.
Harmonize ameongeza kuwa aliamua kutoa ufafanuzi huo hadharani ili kuufahamisha umma ukweli wa jambo hilo, akisema hapo awali baadhi ya watu walikuwa wanamchukulia vibaya kutokana na taarifa zilizokuwa zikisambaa kuhusu mgogoro wao. Kwa sasa, amesema kila upande utaendelea na maisha yake kwa amani.