Entertainment

Jaguar Afichua Ombi la Mwisho la Raila Odinga Kabla ya Kifo Chake

Jaguar Afichua Ombi la Mwisho la Raila Odinga Kabla ya Kifo Chake

Msanii mkongwe wa muziki na mwanasiasa nchini Kenya, Jaguar, amefunguka kuhusu mazungumzo yake ya mwisho na marehemu Raila Amolo Odinga, akieleza kwamba kiongozi huyo alitamani kumwona akitunga wimbo mwingine.

Kupitia ujumbe wake Instagram, Jaguar amesema kuwa alikutana na Raila walipokuwa kwenye ndege moja wakielekea Dubai, wiki chache zilizopita na katika mazungumzo yao, Raila alimwambia wazi kuwa angependa kumsikia tena akiimba wimbo mpya, baada ya kufurahishwa na ukubwa wa “Kigeugeu”, wimbo uliomfanya Jaguar kupata umaarufu mkubwa miaka kadhaa iliyopita.

Msanii huyo amesema ombi hilo lilitolewa kwa utulivu na upole, na hakulijua kuwa lingekuwa mazungumzo ya mwisho kati yake na kiongozi huyo ambaye alimchukulia kama mtu wa mfano na chanzo cha motisha katika safari yake ya muziki.

Jaguar ambaye kwa wakati mmoja alikuwa mbunge wa Starehe, amesema kuwa ombi hilo la kutunga wimbo mpya litabaki kuwa kumbukumbu ya thamani maishani mwake na kwamba atalitumia kama hamasa ya kumuenzi kiongozi huyo mwenye moyo wa upendo na aliyeamini katika vijana na nguvu zao za kubadilisha jamii kupitia sanaa.

Ikumbukwe miaka kumi na minne iliyopita, Raila Odinga alimtambulisha Jaguar hadharani kwenye kipindi cha Churchill Live kama msanii anayempenda zaidi, akimtaja kupitia wimbo wake maarufu wa Kigeugeu, jambo lililomfungulia milango mingi katika muziki na siasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *