Entertainment

John Blaq: Akaunti Yangu ya YouTube Ilichukuliwa kwa Mabavu na Black Market

John Blaq: Akaunti Yangu ya YouTube Ilichukuliwa kwa Mabavu na Black Market

Staa wa muziki kutoka Uganda, John Blaq, amefunguka kuhusu sababu iliyopelekea mashabiki wengi kudhani kuwa aliacha muziki kwa muda. Amedai kuwa hali hiyo ilitokana na mgogoro ulioibuka kati yake na uongozi wa lebo ya Black Market kipindi cha janga la COVID-19.

Kwa mujibu wa msanii huyo, tofauti hizo zilifikia hatua ya kumpokonya akaunti yake ya YouTube ambayo ilikuwa imejikusanyia zaidi ya wafuasi 100,000. Alifafanua kuwa uongozi wa lebo hiyo ulimtaka alipe kiasi cha shilingi milioni 150 ili kurejeshewa akaunti hiyo, jambo ambalo hakuweza kulitekeleza kutokana na changamoto za kifedha wakati huo.

John Blaq alisema kutokana na hali hiyo alilazimika kuanzisha kituo kipya cha YouTube, hatua iliyowafanya mashabiki wake wengi kudhani kuwa alikuwa ameweka kando muziki. Pia alibainisha kwamba hakuwahi kusaini mkataba rasmi na Black Market, bali walishirikiana kama ndugu katika kazi. Hata alipojaribu kutafuta maridhiano, juhudi zake hazikufanikiwa baada ya upande huo kukataa suluhu.

Licha ya changamoto hizo, John Blaq amesema hakuwahi kufikiria kuacha muziki. Kwa sasa anafanya vizuri na albamu yake mpya African Buoy yenye jumla ya nyimbo 15, ambapo amewashirikisha wasanii kama Maro, Skales, Laika na wengine wengi. Albamu hiyo imepokelewa vizuri na mashabiki, ikionesha kuwa msanii huyo bado anaendelea kuimarisha nafasi yake katika muziki wa Afrika Mashariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *