Miamba wa soka nchini Italia, Juventus, wametangaza kumfuta kazi kocha wao Igor Tudor kufuatia msururu wa matokeo duni uliomalizika kwa kichapo cha 3-0 dhidi ya Lazio Jumapili iliyopita.
Kocha huyo raia wa Croatia, mwenye umri wa miaka 43, alijiunga na Juventus mwezi Machi kuchukua nafasi ya Thiago Motta, lakini ameshindwa kuipa timu matokeo chanya. Tangu achukue usukani, Juventus imepoteza mechi nane mfululizo, hali iliyowaacha katika nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi ya Serie A.
Kichapo dhidi ya Lazio kilikuwa cha tatu mfululizo kwa timu hiyo katika mashindano yote, na kimechochea uamuzi wa uongozi wa klabu kumtimua kocha huyo.
Kupitia taarifa rasmi, Juventus imetangaza kuwa Massimiliano Brambilla atachukua majukumu ya muda na kuiongoza timu kwenye mechi ijayo ya Serie A dhidi ya Udinese.
Kwa sasa, Juventus wana alama sita nyuma ya vinara Napoli, wakiwa wamepoteza mechi tano zilizopita za ligi. Aidha, katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, klabu hiyo inashikilia nafasi ya 25 kwenye msimamo wa makundi baada ya kupoteza mechi moja na kutoka sare mara mbili katika mechi tatu za mwanzo.
Hatua hii inaonekana kama jaribio la kuokoa msimu wa Juventus ambao umetikiswa na matokeo mabaya na ukosefu wa uthabiti tangu mwanzo wa mwaka huu.