
Msanii na mwigizaji wa Kenya, Habida, amefunguka kwa uchungu kuhusu tukio la kusikitisha zaidi kuwahi kumkumba maishani, akieleza kwa ujasiri kuwa aliwahi kubakwa na kwamba haoni haja ya kuficha ukweli huo.
Katika mahojiano ya kina yaliyogusa hisia za wengi kupitia podcast ya SPM Buzz, Habida alisema kuwa bado haelewi kwa nini alitendewa ukatili huo, akisisitiza kuwa hakufanya jambo lolote lililostahili adhabu ya aina hiyo.
“Sikufanya chochote kilichompa haki ya kunitendea vile. Nilinyanyaswa kingono. Nimewahi kubakwa. Sifichi, kwa sababu hiyo ni sehemu ya safari yangu,” alisema kwa sauti ya utulivu lakini yenye uzito mkubwa.
Habida alieleza kuwa kwa muda mrefu alibeba uzito wa kimya, lakini amejifunza kuwa kunyamaza huongeza maumivu na kumzuia mtu kupona. Sasa anatumia sauti yake kuwahamasisha wanawake na wanaume waliopitia unyanyasaji wa aina hiyo, kuzungumza na kutafuta msaada.
“Najua kuna watu wengi waliopitia haya kama mimi. Nataka wajue hawako peke yao. Hatupaswi kuaibika kwa majeraha yaliyotusababishiwa na wengine,” aliongeza.
Kauli ya Habida imeibua mjadala mpana mitandaoni kuhusu ukatili wa kijinsia na jinsi jamii inavyoshughulikia waathirika wa matukio hayo. Wengi wamepongeza ujasiri wake na kumtia moyo kwa kuchukua hatua ya kuongea hadharani, wakiitaka jamii iwe na huruma zaidi na kujenga mazingira salama kwa waathirika kutoa ushuhuda wao.
Habida, anayejulikana kwa sauti yake ya kipekee na mchango wake mkubwa katika muziki wa Kenya, anaendelea kutumia jina lake kushawishi mabadiliko ya kijamii na kuinua wale waliovunjwa moyo kimya kimya.