Mwanaharakati Lillian Ng’ang’a amejiunga na mjadala unaoendelea mtandaoni kuhusu kundi la waimbaji wa injili na influencers kutoka Kenya walioitikia mwito wa kusafiri nchini Israel kupitia kampeni ya utalii ya “Israel in Kenya.”
Kupitia Instastory yake, Lillian Ng’ang’a amewakingia kifua wasanii na influencers hao, akibainisha kuwa ziara yao haihusiani na msimamo wa kisiasa wala kuunga mkono upande wowote kwenye vita vinavyoendelea Gaza.
Lillian Ng’ang’a amesisitiza kuwa kutembelea Israel hakumaanishi kwamba influencers hao hawana huruma kwa Wapalestina.
Ameongeza kuwa Israel ni nchi ambayo watu wengi wamekuwa wakitamani kuitembelea kwa sababu za kiimani na kihistoria na si kwa sababu za kisiasa. Mwanamama huyo, amemalizia ujumbe kwa kusema kuwa watu wanapaswa kutenganisha safari za utalii na propaganda za kivita.
Kauli ya Lilian imekuja mara baada ya baadhi ya Wakenya kukosoa safari hiyo, wakidai kuwa kutangaza Utalii wa Israel wakati mgogoro wa Israel–Gaza ukiendelea ni hatua isiyo na utu na inaweza kuonekana kama kuunga mkono vita.
Mastaa waliojumuisha kwenye safari hiyo ni pamoja na Mwende Macharia, Kambua, Evelyn Wanjiru na mumewe Agundabweni Akweyu, Jasmine Mungai, Mimo Karanja, Kestine Mbogo, Bona Bismack Okello, Salimo wa Kilimo, Susan Grace na Gadwilliam Kiragu Kimani. Safari hiyo iligharamia kikamilifu usafiri wa ndege, malazi na chakula, bila malipo ya pesa taslimu kwa washiriki.