Mwanaharakati wa masuala ya kijamii nchini Kenya, Lillian Ng’ang’a, ameibua mjadala muhimu kuhusu ongezeko la vijana wa kike wanaokimbilia kufanya taratibu hatarishi za urembo, akiwataka kuzingatia njia za asili na salama za kujitunza.
Kupitia ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, Ng’ang’a ameeleza wasiwasi wake kuhusu mwenendo unaozidi kushika kasi ambapo wanawake wanatumia kemikali na upasuaji ili kubadilisha maumbile yao.
Lillian amesema kuwa kuna haja ya wanawake kujenga uelewa kwamba mwonekano wa kudumu na wenye afya hauwezi kupatikana kupitia njia za mkato. Ameonya kuwa suluhisho la haraka mara nyingi huja na madhara ya muda mrefu kiafya.
Hata hivyo amesisitiza kuwa lishe bora, mazoezi ya mwili na kujikubali ndivyo vinavyoweza kujenga mwili wenye afya bila kuhatarisha maisha.