Sports news

Matokeo ya EPL: Arsenal Waang’ara, United na Chelsea Wasalimu Amri kwa Sare

Matokeo ya EPL: Arsenal Waang’ara, United na Chelsea Wasalimu Amri kwa Sare

Ligi Kuu ya England iliendelea hapo jana kwa michezo kadhaa iliyopigwa katika viwanja tofauti, na matokeo yake yalileta taswira mpya kwenye mbio za ubingwa.

Manchester United walibanwa nyumbani na Wolves kwa sare ya 1-1. Bao la Zirkzee dakika ya 27 liliwapa mashabiki wa Old Trafford matumaini, lakini Krejci akasawazisha kabla ya mapumziko na kuondoa furaha hiyo.

Washika Mitutu, Arsenal, waliendeleza ubabe wao kwa kuichapa Aston Villa 4-1 katika dimba la Emirates. Gabriel alifungua ukurasa wa mabao dakika ya 48, Zubimendi akaongeza la pili dakika ya 52, kisha Trossard na Jesus wakahitimisha karamu ya mabao. Watkins alifuta machozi kidogo kwa Villa dakika ya 90+4, lakini haikutosha kuzuia kipigo kizito.

Chelsea nao walibanwa Stamford Bridge na AFC Bournemouth kwa sare ya 2-2. Palmer alifunga kwa penalti dakika ya 15, Fernandez akaongeza la pili dakika ya 23, lakini Brooks na Kluivert walihakikisha Bournemouth wanatoka na alama moja muhimu.

Katika mechi nyingine, Burnley walichapwa 3-1 na Newcastle United, West Ham wakalazimishwa sare ya 2-2 na Brighton, huku Nottingham Forest wakipigwa 2-0 na Everton.

Kwa matokeo haya, Arsenal wamepanda kileleni mwa msimamo wakiwa na pointi 45, wakiacha pengo la alama 5 dhidi ya Manchester City walioko nafasi ya pili na pointi 40. Wapinzani wao wakuu kama United na Chelsea walibanwa nyumbani na kupoteza nafasi ya kupunguza tofauti, jambo linalozidi kuimarisha matumaini ya Washika Mitutu kutwaa ubingwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *