Mwanamuziki nyota wa Rhumba kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mbilia Bel, ameungana na Wakenya kuomboleza kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Amolo Odinga.
Kupitia mitandao ya kijamii, Mbilia Bel ametuma salamu za pole kwa familia ya hayati Odinga, hasa mjane wa kiongozi huyo Mama Ida, akieleza kuguswa sana na msiba huo mkubwa unaoigusa taifa la Kenya na bara zima la Afrika.
Mbilia Bel, anayefahamika kwa sauti yake nyororo na mitindo ya kucheza yenye mvuto wa kipekee, amesema Raila alikuwa kiongozi mwenye heshima, upendo, na anayethamini sana sanaa na wasanii kutoka mataifa mbalimbali, ikiwemo Kongo.
Mama Afrika, ameongeza kuwa anaikumbuka Kenya kwa mapenzi makubwa, akisema ni moja ya mataifa yaliyompa jukwaa kubwa zaidi katika miaka ya 1980 na 1990 alipokuwa kileleni mwa umaarufu wake.
Kwa Wakenya wengi, Mbilia Bel amekuwa nembo ya muziki wa Afrika wa kizazi cha dhahabu, na nyimbo zake kama Nakei Nairobi na Nadina zimeendelea kupendwa hadi leo kwenye vituo vya redio na hafla mbalimbali.
Lakini pia ni moja kati ya wasanii wa kike barani Afrika aliyefanya ziara kadhaa nchini humo, akitumbuiza katika miji ya Nairobi, Mombasa, na Kisumu, na kujizolea umaarufu mkubwa miongoni mwa wapenzi wa Rumba.