Makala ya 2025 ya mbio za basikeli barani Afrika yalianza leo kwenye uwanja wa Absa Diani, kaunti ya Kwale. Kiros Tsige wa Ethiopia aliibuka mshindi kwenye mashindano ya mbio za kilomita 14 baada ya kuadikisha muda wa dakika 10 nasekunde 56.979.
Alifuatwa na Tesfu Adyam wa Eritrea kwa muda wa dakika 11 na sekunde 02.866 ilihali Yvonne Masengesho wa Rwanda akimaliza wa tatu kwa dakika 11 sekunde 20.561.
Hata hivyo waakilishi wa kenya Jepkorir Mercy na Sharon Cheruiyot walikosa kumaliza katika nafasi za tano bora baada ya kuchukua nafasi za kumi na kumi na mbili mtawalia.
Katika mashindano ya wavulana, Hardy Tristan wa Mauritius alitwaa ushindi kwa muda wa dakika 9 na sekunde 24.64 ilihali Efriem Nahom wa Eritrea na Woolley Dean wa Afrika kusini wakimaliza wa pili na tatu mtawalia.