
Mtangazaji wa redio Mkamburi Chigogo ameibua mjadala mkali baada ya kuwakejeli baadhi ya mabalozi wa mitandaoni nchini wanaofanyiwa upasuaji wa urembo.
Kupitia ujumbe alioutoa, Mkamburi amedokeza kuwa licha ya gharama kubwa zinazotumika, matokeo ya upasuaji huo mara nyingi hayaonekani kuwa na tofauti kubwa. Ametania kwa kusema kuwa ni nchini Kenya pekee ambapo mtu akifanyiwa upasuaji wa urembo, anabaki namna alivyokuwa awali bila mabadiliko yoyote.
Kauli hiyo imeibua hisia mseto mitandaoni, huku baadhi ya wafuasi wakihusisha ujumbe wake na mrembo Pritty Vishy, ambaye hivi karibuni alionesha picha zake za kabla na baada ya kufanyiwa mchakato wa kuongeza makalio (BBL), kuondoa mafuta ya ziada mwilini (liposuction), na kupunguza ngozi na mafuta tumboni (tummy tuck).
Wafuasi wake wamegawanyika, baadhi wakikubaliana naye wakisema mabadiliko hayo mara nyingi hufanywa kwa kutafuta kiki, ilhali wengine wakimtuhumu kwa kejeli na kutetea kwamba kila mtu ana uhuru wa kufanya maamuzi kuhusu mwili wake.