Mkenya Ruth Jepchumba Bundotich ametajwa kuwa Mwanamke Bora wa Shirikisho la Riadha Duniani mwaka 2025, na kutunukiwa tuzo maalum kutokana na mchango wake mkubwa katika uongozi na maendeleo ya riadha.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Riadha Duniani, Bundotich ametambuliwa kwa uongozi wake shupavu, kujitoa kwake kwa mustakabali wa wanariadha, na juhudi za kubadilisha taswira ya riadha ya wanawake nchini Kenya na kimataifa.
Kazi yake kupitia Wakala wa Michezo wa Ikaika pamoja na Adidas Running imeelezwa kuwa msingi muhimu katika kujenga mfumo endelevu wa kuwalea na kuwaendeleza wanariadha chipukizi.
Shirikisho hilo limesema kuwa juhudi za Bundotich zimewezesha wasichana wengi kupata mafunzo, msaada, na mazingira salama ya kuendeleza vipaji vyao ndani na nje ya uwanja.
Miongoni mwa matunda ya kazi yake ni kuinukia kwa nyota kama Agnes Ngetich, mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 10.