
Msanii maarufu wa muziki wa Gengetone, Parroty, ameibua mjadala mkali baada ya kuwakosoa vikali watu maarufu nchini Kenya kwa kutochukua msimamo kuhusu changamoto za kijamii zinazolikumba taifa.
Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa Instagram, Parroty alieleza kusikitishwa na kile alichokiita kupuuza kwa makusudi matatizo ya wananchi na kuweka mbele maslahi binafsi. Alisema kuwa kuna ongezeko la wasanii, wachekeshaji, wanamitandao maarufu na wanamichezo ambao wanachagua kukaa kimya kuhusu masuala nyeti kama umasikini, ukosefu wa haki, ufisadi, na ukatili wa polisi, wakijikita zaidi katika maisha ya anasa na biashara binafsi.
Kwa mujibu wa Parroty, watu maarufu wamekuwa wakitumia majukwaa yao kwa malengo ya kibinafsi badala ya kuhamasisha mabadiliko ya kijamii. Alielezea kuwa hali hiyo imesababisha mwanya mkubwa kati yao na mashabiki wanaowategemea kama sauti ya mabadiliko.
Katika ujumbe wake, Parroty alitumia maneno makali kuwaelezea watu maarufu wanaoweka mbele matumbo yao kuliko utu na haki za wananchi. Alisisitiza kuwa umaarufu unapaswa kutumika kama jukwaa la kuhamasisha jamii na kushinikiza mabadiliko chanya.
Kauli yake imekuja katika kipindi ambapo taifa linakumbwa na hasira kufuatia kifo cha bloga Albert Ojwang, aliyeripotiwa kufariki akiwa mikononi mwa polisi. Tukio hilo limezua maandamano na hisia kali miongoni mwa wananchi waliotaka uwajibikaji na haki kutendeka.
Ujumbe wa Parroty umeungwa mkono na sehemu kubwa ya wananchi mitandaoni, wengi wao wakielezea kuwa ni wakati muafaka kwa watu mashuhuri kuacha kukaa kimya na kuchukua hatua madhubuti katika kupigania ustawi wa jamii.