Entertainment

Parroty Vunulu Alalamikia Redio za Kenya Kupendelea Wasanii wa Tanzania

Parroty Vunulu Alalamikia Redio za Kenya Kupendelea Wasanii wa Tanzania

Msanii wa muziki wa Gengetone Parroty Vunulu ameibuka na malalamiko makali dhidi ya baadhi ya vituo vya redio nchini Kenya, akidai vinapendelea wasanii wa Tanzania huku vikisahau kabisa kukuza na kuunga mkono wasanii wa ndani.

Kupitia mitandao yake ya kijamii, Parroty Vunulu amesema redio nyingi za Kenya zimekuwa zikijikita zaidi katika kuzungumzia na kupiga muziki wa wasanii wa nje, hasa kutoka Tanzania, huku zikiongelea matukio na mafanikio yao mara kwa mara kwenye vipindi mbalimbali. Kwa mujibu wake, hali hiyo inawanyima nafasi wasanii wa Kenya ambao pia wanajitahidi kuandaa kazi na matukio yenye mvuto mkubwa.

Msanii huyo ameeleza kuwa licha ya wasanii wa ndani kuendelea kutengeneza matukio, kuachia nyimbo mpya na kufanya juhudi za kuinua tasnia ya muziki wa Kenya, watangazaji wengi wamekuwa wakipuuza juhudi hizo kwa kutozizungumzia wala kuzipa nafasi inayostahili hewani.

Parroty Vunulu ametoa onyo kali kwa redio hizo akizitaka zibadilishe mwelekeo wao na kuanza kudhamini, kupigia debe na kuzungumzia muziki wa Kenya pamoja na wasanii wake. Ameonya kuwa endapo hali hiyo itaendelea, basi Wakenya wanafaa kufikiria kususia kusikiliza redio ambazo hazithamini na kuunga mkono muziki wa ndani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *