Rais Samia Suluhu Hassan ameipongeza timu ya soka ya Tanzania Taifa Stars kwa kufuzu kwa mechi za 16 bora kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Morocco huku akieleza kuwa mafanikio hayo ni ya kihistoria na ni fahari kubwa kwa taifa hilo.
Taifa Stars ilifanikiwa kufuzu kwa mechi za mwuondoano kwa mara ya kwanza baada ya miaka 45 baada ya kuwabana Tunisia kwa sare ya bao 1-1 mjini Rabat. Matokeo hayo yameifanya Tanzania kusonga mbele ikiwa ni miongoni mwa timu bora zilizomaliza katika nafasi ya tatu.
Tanzania ilimaliza katika nafasi ya tatu katika Kundi C ikiwa na alama mbili, ikiishinda Angola, ambayo pia ilikuwa na alama mbili lakini iliondolewa mashindanoni kwa ubora wa mabao.
Taifa Stars itaanza harakati zake za kuwania kufuzu kwa mechi za robo fainali Jumapili hii itakapomenyana na wenyeji Morocco kwenye Uwanja wa Prince Moulay Abdellah mjini Rabat.