Bifu kati ya mtangazaji wa Kenya, Rapcha the Sayantist, na rapa nyota, Khaligraph Jones, limechukua mkondo mpya baada ya Rapcha kudai kuwa Khaligraph aliwahusisha polisi katika mgogoro wao.
Mzozo huu ulianza baada ya Rapcha, kupitia podcast yake, kumtaja Khaligraph kama msanii feki, akipinga lafudhi yake, asili yake ya Kayole, mtindo wa rap na uhalisia wa kazi zake za muziki. Kauli hizo zilichochea mjadala mkali mitandaoni na kugawanya mashabiki wa hip hop Afrika Mashariki.
Khaligraph alipuuza shutuma hizo akizihusisha na mbinu za kutafuta kiki, na akamtangaza Rapcha kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii kwa mtindo wa kebehi, akionesha kuwa hatambui hoja zilizotolewa.
Hata hivyo, mambo yalichukua sura mpya baada ya Rapcha kudai kuwa Khaligraph alihusisha polisi ili kuzima bifu hilo. Kwa mtangazaji huyo, hatua ya kupeleka mgogoro wa muziki kwa vyombo vya usalama ilikuwa ni ishara ya udhaifu na kutojiamini katika kukabiliana na changamoto za kisanaa. Alieleza kuwa tabia ya aina hiyo inaua roho ya hip hop, kwa sababu badala ya kujibu hoja kwa ubunifu au kuendeleza mashindano ya kisanaa, wasanii wakubwa wanatumia nguvu zao kuwakandamiza wanaowakosoa.
Mashabiki wameendelea kutofautiana, baadhi wakimtetea Khaligraph kama msanii mwenye hadhi ya kimataifa asiye na ulazima wa kujibu kila ukosoaji, huku wengine wakimpongeza Rapcha kwa uthubutu na kuibua mijadala mipya katika tasnia ya muziki.
Mpaka sasa, Khaligraph hajajibu moja kwa moja madai ya kuhusisha polisi. Wachambuzi wa burudani wanasema bifu hili linaweza kubaki kama mjadala wa kawaida wa mitandaoni au kugeuka kuwa mvutano mkubwa unaoweza kuathiri taswira ya hip hop Afrika Mashariki.