Timu ya Taifa ya Senegal imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 baada ya kuifunga Morocco bao 1-0 katika mchezo wa fainali uliochezwa mjini Rabat.
Mchezo huo ulimalizika kwa sare ya bila mabao katika dakika 90 za kawaida. Dakika ya 90 Morocco walipata nafasi ya penati, lakini mchezo ulisimama kwa takribani dakika 10 baada ya wachezaji wa Senegal na benchi la ufundi kugomea mkwaju huo na kuondoka uwanjani. Baada ya kurejea, Morocco walikosa nafasi hiyo muhimu.
Senegal ilipata bao la ushindi dakika ya 94 kupitia Pape Gueye, na kufanikisha kutwaa taji lao la pili la AFCON. Mara ya kwanza walibeba kombe hilo mwaka 2021.
Kwa upande wa Morocco, hii ilikuwa nafasi ya pili kufika fainali tangu walipotwaa ubingwa wao wa pekee mwaka 1976.
Ushindi huu unaimarisha hadhi ya Senegal kama moja ya timu kubwa barani Afrika, huku Morocco ikibaki na kumbukumbu ya kupoteza fainali mbele ya mashabiki wao nyumbani.