
Watumiaji wa Spotify ambao hawalipi ada ya kila mwezi sasa wamepata habari njema baada ya kampuni hiyo kupanua huduma zake. Kwa sasa, watumiaji wa Spotify ya Bure wanaweza kucheza nyimbo wanazozitaka moja kwa moja kupitia playlists, albums, na hata kwenye profiles za wasanii.
Hapo awali, mfumo wa bure ulikuwa na vizuizi kadhaa ambavyo vilikuwa vikiwalazimisha watumiaji kusikiliza nyimbo kwa mtindo wa “shuffle” pekee, na hivyo kuwanyima uhuru wa kuchagua moja kwa moja wimbo wanaoutaka.
Hatua hii mpya inatazamwa kama jitihada za Spotify kuongeza idadi ya watumiaji wake na kuwapa uzoefu bora zaidi, huku ikishindana na majukwaa mengine ya muziki kama vile Apple Music, YouTube Music na Boomplay.
Wataalamu wa teknolojia wanasema mabadiliko haya yanaweza kuongeza mvuto wa watumiaji wapya na kuwashawishi baadaye kujiunga na mpango wa kulipia ili kufurahia huduma za ziada kama vile kusikiliza muziki bila matangazo na kupakua nyimbo.
Spotify, ambayo kwa sasa ni moja ya majukwaa makubwa zaidi ya kusikiliza muziki duniani, inaendelea kuboresha huduma zake ili kuendana na mahitaji ya wapenzi wa muziki katika kila kona ya dunia