Msanii wa muziki kutoka Kenya, Stevo Simple Boy, amekanusha madai kwamba aliwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mrembo aitwaye Pritty Vishy, akieleza kuwa mahusiano yao yaliishia katika hatua ya mazungumzo (talking stage).
Akizungumza kwenye podcast ya AM, Stevo amesema kuwa licha ya kuwa mwaminifu katika mapenzi, aligundua kuwa Pritty hakuwa na nia njema katika uhusiano huo, bali alikuwa na malengo yake binafsi.
Stevo ambaye anafanya vizuri na wimbo wake mpya uitwao Fanana, ameeleza kuwa baada ya kutengana, Pritty alianza kuzungumza mambo mabaya kumhusu, lakini yeye alichagua kubaki kimya ili kuepuka kuendeleza mizozo ya mtandaoni.
Stevo ameongeza kuwa anamshukuru Mungu kwa kuhifadhi ubikra wake hadi alipompata mke anayempenda na kumjali kwa dhati. Msanii huyo pia amefichua kuwa wanatarajia kupata mtoto wao wa kwanza hivi karibuni, hatua anayosema ni baraka kubwa katika maisha yake.