Ivory Coast na Algeria Zatinga Robo Fainali AFCON 2025
Timu ya Taifa ya Ivory Coast, maarufu kama The Elephants, imefanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Burkina Faso katika mchezo wa hatua ya 16 bora. Katika mchezo huo, Ivory Coast ilionyesha ubora mkubwa tangu mwanzo, ambapo Amad Diallo alifungua ukurasa wa mabao dakika ya 20. Yan Diomande aliongeza bao la pili dakika ya 32, kabla ya mchezaji wa akiba Bazoumana TourΓ© kufunga bao la tatu dakika ya 87 na kukamilisha ushindi huo mnono kwa The Elephants. Wakati huo huo, Timu ya Taifa ya Algeria nayo imefuzu robo fainali baada ya kuiondoa DR Congo kwa ushindi wa bao 1-0 katika mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa na wa kusisimua. Mchezo huo ulimalizika bila mabao ndani ya dakika 90 za kawaida, hali iliyosababisha kuchezwa kwa muda wa nyongeza. Bao la ushindi kwa Algeria lilifungwa na mchezaji wa akiba Adil Boulbina dakika ya 119 ya mchezo, kwa shuti kali lililowashangaza walinzi na kipa wa DR Congo, na kuwapeleka The Desert Foxes hatua ya nane bora. Kutokana na matokeo hayo, Ivory Coast sasa itavaana na Egypt katika mchezo wa robo fainali, huku Algeria ikitarajiwa kupambana vikali na Nigeria. Mechi hizo za robo fainali zinatarajiwa kuchezwa Jumamosi.
Read More