Gloria Bugie Akiri Mwili Wake Sio Hekalu la Mungu
Msanii wa muziki kutoka Uganda, Gloria Bugie, amezua mjadala mpana baada ya kukiri wazi kuwa mwili wake sio hekalu la Mungu, akisema amefanya dhambi nyingi katika maisha yake ya nyuma. Gloria Bugie amesema kuwa amewahi kuingia katika mahusiano ya kimapenzi na watu wenye ushawishi mkubwa ndani ya tasnia ya burudani. Kwa mujibu wake, mahusiano hayo yalichangia kwa kiasi kikubwa kufunguka kwa milango ya fursa, hususan kupata mikataba mikubwa ya kazi, tofauti na mafanikio aliyoyapata kupitia muziki wake pekee. Amesema kuwa wakati huo alifanya maamuzi ambayo hakuyapima kwa misingi ya imani au maadili, akieleza kuwa alikuwa akitafuta njia za haraka za kufanikiwa na kujijenga kimaisha. Gloria Bugie ameongeza kuwa hakujiona kama alikuwa anajidharau, bali alikuwa akifanya kile alichoona ni njia ya kujinusuru katika mazingira magumu ya ushindani mkubwa kwenye tasnia. Hata hivyo, kauli hizo zimeibua hisia mseto miongoni mwa watumiaji wa mitandao ya kijamii, ambapo baadhi wamempongeza kwa ujasiri wa kusema ukweli wake bila kuficha, huku wengine wakimkosoa vikali wakidai kauli hizo zinaweza kuhamasisha mmomonyoko wa maadili, hasa kwa vijana.
Read More