Irene Uwoya Akanusha Kuwahi Kufunga Ndoa na Dogo Janja
Muigizaji mkongwe wa filamu za Bongo, Irene Uwoya, amekanusha vikali madai kuwa aliwahi kufunga ndoa na msanii wa muziki pamoja na Diwani wa Kata ya Ngarenaro, Abdulazizi Chande maarufu kama Dogo Janja. Uwoya, ambaye kwa sasa amejikita zaidi katika huduma za kiroho kama mchungaji, amesema wazi kuwa hakuna cheti chochote cha ndoa kinachothibitisha kuwa aliwahi kuoana na Dogo Janja. Kauli hiyo imekuja licha ya baadhi ya waigizaji wenzake kudai kuwa aliwahi kuwaonyesha cheti hicho kipindi cha nyuma. Akizungumza kwenye Reality Show ya A List ya wasanii wa kike wa Bongo Movie, Uwoya amesisitiza kuwa ndoa pekee anayoitambua na kuifahamu rasmi ni ile aliyofunga kanisani na marehemu mume wake, akieleza kuwa hiyo ndiyo ndoa ya kweli na halali kwake mbele za Mungu na jamii. Kauli ya Irene Uwoya imeibua mjadala mpana mitandaoni, hasa miongoni mwa mashabiki wa burudani, wakijaribu kufahamu ukweli wa mahusiano yake ya zamani na Dogo Janja pamoja na msimamo wake wa sasa baada ya kugeukia maisha ya kiimani. Ikumbukwe Irene Uwoya na Dogo Janja walifunga ndoa mwaka 2017, ingawa baadaye ndoa hiyo ilivunjika na wawili hao wakaachana kwa amani.
Read More