AK Yatoa Ratiba ya Msimu Mpya wa Riadha

AK Yatoa Ratiba ya Msimu Mpya wa Riadha

Chama cha Riadha Nchini (AK) kimetoa ratiba rasmi ya msimu ujao wa mbio na fani mbalimbali za riadha za uwanjani, ambapo msimu huo unatarajiwa kuanza rasmi wikendi hii katika uwanja wa Mumias. Kulingana na taarifa iliyotolewa na chama hicho, hatua ya kutoa ratiba mapema inalenga kuwapa wanariadha muda wa kutosha kujiandaa vyema kabla ya kushiriki katika mashindano ya kimataifa. Baada ya kufanyika kwa duru ya kwanza Mumias, mashindano hayo yataendelea mjini Kapsabet kuanzia Machi 14 hadi 16, kisha kufuata na Afraha Stadium, Nakuru, Machi 27–28. Mikondo miwili ya mwisho ya msururu huo itaandaliwa mwezi Mei katika viwanja vya Nyayo na Ulinzi jijini Nairobi, ambapo duru hizo zitawahusisha wanariadha watakaoalikwa pekee kutokana na ushindani wake wa juu. Wanariadha wa Kenya wanatarajiwa kutumia mashindano hayo kama maandalizi muhimu kuelekea Michezo ya Jumuiya ya Madola yatakayofanyika mjini Glasgow mwezi Agosti mwaka ujao. Kenya inalenga kuboresha matokeo yake ya toleo la mwisho lililofanyika mjini Birmingham mwaka 2022, ambapo ilishika nafasi ya tatu kwa kupata jumla ya nishani 20; sita za dhahabu, tano za fedha na tisa za shaba.

Read More