MC Pilipili Azikwa katika Makaburi ya Kilimo Kwanza, Dodoma
Mchekeshaji na mshereheshaji wa matukio Emmanuel Mathias Matebe, maarufu kama MC Pilpili, amepumzishwa kwenye nyumba yake ya milele katika makaburi ya Kilimo Kwanza jijini Dodoma leo, Novemba 20, 2025. Mamia ya waomboleza, wakiwemo wasanii, ndugu, marafiki na viongozi wa dini, walijitokeza kumuaga mchekeshaji huyo aliyekuwa akipendwa na wengi kutokana na kipaji chake cha kuiburudisha jamii. MC Pilpili, ambaye pia alijulikana kwa mchango wake katika tasnia ya filamu na uigizaji, ameacha pengo kubwa katika burudani ya Tanzania. Waomboleza waliohudhuria mazishi yake walimkumbuka kama mtu mcheshi, mnyenyekevu na mwenye uwezo wa kuleta tabasamu nyusoni mwa watu katika nyakati zote. MC Pilpili aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana Jumapili ya Novemba 16, 2025 akiwa jijini Dodoma. Tukio hilo lilisababisha simanzi kubwa nchini Tanzania, huku mashabiki na wadau wa sanaa wakishinikiza haki itendeke na wahusika wafikishwe mbele ya sheria. Jeshi la Polisi limeendelea na uchunguzi kuhusu mauaji hayo, likikusanya vielelezo na ushahidi ili kubaini watu waliohusika. Maafisa wa upelelezi wamesema kuwa jitihada za kusaka wahalifu zinaendelea kwa kasi na umma utaarifiwa pindi hatua muhimu zitakapofikiwa.
Read More