MozzartBet Yadhamini Shirikisho la Mpira wa Wavu kwa KSh 15 Milioni

MozzartBet Yadhamini Shirikisho la Mpira wa Wavu kwa KSh 15 Milioni

Shirikisho la mchezo wa mpira wa wavu nchini Kenya (KVF) limepokea udhamini wa shilingi milioni 15 kutoka kampuni ya michezo ya kubashiri ya MozzartBet, katika hafla fupi iliyofanyika jijini Nairobi. Hafla hiyo ilihudhuriwa na kinara wa Shirikisho la Mpira wa Wavu Barani Afrika (CAVB), Bouchra Hajij, ambaye yuko nchini kwa ziara rasmi ya kikazi. Akizungumza wakati wa uzinduzi wa udhamini huo, mwenyekiti wa KVF Charles Nyaberi ameishukuru MozzartBet kwa kuendelea kuwa mdau muhimu katika maendeleo ya mpira wa wavu nchini. Amesema kampuni hiyo imekuwa ikitoa mchango mkubwa kwa timu za taifa Malkia Strikers (wanawake) na Wafalme (wanaume) ambazo zimeweka Kenya kwenye ramani ya michezo ya kimataifa. Kwa upande wake, Rais wa CAVB Bouchra Hajij ameipongeza Kenya kwa juhudi zake katika kukuza mchezo wa mpira wa wavu na akatoa mwito kwa mashirikisho ya kitaifa barani Afrika kuwekeza zaidi katika maendeleo ya wachezaji wa ngazi za chini. Udhamini huo wa KSh 15 milioni unatarajiwa kupunguza mzigo wa kifedha kwa KVF na kusaidia maandalizi ya timu za taifa kushiriki kikamilifu kwenye michuano ijayo ya kimataifa, huku ukichangia pia katika kukuza na kuimarisha mchezo wa mpira wa wavu nchini.

Read More