Nairobi United Kutafuta Heshima kwenye Kombe la Shirikisho Afrika
Timu ya ligi kuu ya FKF, Nairobi United, imetengwa katika kundi B la michuano ya kuwania Kombe la Mashirikisho barani Afrika (CAF Confederation Cup) kufuatia droo iliyoandaliwa jana jioni jijini Johannesburg, Afrika Kusini. Nairobi United itakuwa na kibarua kigumu kwani itachuana na Azam FC kutoka Tanzania, AS Maniema Union ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, pamoja na Wydad Casablanca, miamba wa soka kutoka Morocco. Michuano hiyo inatarajiwa kuanza rasmi tarehe 21 mwezi huu, huku awamu ya mwondoano (knockout stage) ikipangwa kuanza tarehe 13 Machi 2026. Katika droo hiyo, kundi A linajumuisha USM Alger (Algeria), Djoliba AC (Mali), OC Safi (Morocco) na San Pedro (Côte d’Ivoire). Kundi C linaundwa na CR Belouizdad, Stellenbosch FC, AS Otoho na Singida Fountain Gate kutoka Tanzania. Kundi D, linalotajwa kuwa la “mauti”, linashirikisha Zamalek, Al Masry, Kaizer Chiefs, na Zesco United. Kwa mujibu wa kanuni za mashindano, timu mbili bora kutoka kila kundi zitafuzu kwa hatua ya robo fainali, zikifungua ukurasa mpya wa mchuano wa kusaka taji la heshima la klabu bingwa wa Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Read More