Mahakama Yakataa Kuondoa Video ya Utata ya Robert Burale
Mhubiri mwenye utata nchini Kenya Robert Burale amepata pigo kubwa baada ya mahakama ya Nairobi kukataa ombi lake la kutaka mahojiano ya video yaliyofanywa na mke wake wa zamani, Rozina Mwakideu, yafutwe na kuondolewa kwenye mitandao ya kijamii. Katika uamuzi uliotolewa Jumanne,Mahakama imekataa ombi hilo la kuondoa video hiyo mtandaoni, lakini ikaamuru Rozina na Alex Mwakideu kuacha kuchapisha au kusambaza tena mahojiano hayo yenye utata. Hakimu mkaazi wa mahakama ya Milimani, Thomas Nzyoki, amesema kuwa amri iliyotolewa ni ya muda na inalenga kuzuia uchapishaji wowote mpya wa video hiyo kwenye mitandao ya kijamii hadi kesi itakaposikilizwa na kuamuliwa. Amefafanua pia kuwa hatua hiyo haiathiri video ambayo tayari ipo mtandaoni. Wakili anayewakilisha Rozina na Alex Mwakideu, Ochiel Dudley, ameiambia mahakama kuwa wateja wake wataheshimu kikamilifu maagizo yaliyotolewa. Kesi hiyo itatajwa tena tarehe 25 Februari 2026 ili kuhakikisha kuwa pande zote zimewasilisha hoja zao za maandishi. Pasta Burale aliwashtaki Rozina na Alex akiwatuhumu kwa kumdhalilisha (defamation) na kudai fidia ya shilingi milioni 20 za Kenya, akitaka pia mahakama iamuru video hiyo iondolewe mtandaoni na washtakiwa kuomba msamaha hadharani.
Read More 
								