Msanii wa hiphop Frida Amani ameandika historia baada ya kutangazwa rasmi kuwa balozi wa kimataifa unaolenga kulinda, kurejesha na kuimarisha mazingira.
Katika salamu zake za kukubali uteuzi huo, Frida Amani ameweka wazi kuwa anauchukulia kama heshima kubwa na wajibu mzito. Amesisitiza kuwa mazingira ni msingi wa ustawi wa binadamu, na kuzorota kwa hali ya ikolojia kumempa msukumo wa kuchukua hatua za dhati.
Lakini pia ameishukuru Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP kwa kutambua mchango wa wasanii na vijana katika mabadiliko chanya ya kimazingira. Ameahidi kutumia jukwaa lake kuelimisha na kuhamasisha jamii kuhusu ulindaji wa mazingira.
Frida Amani sasa anatarajiwa kuhamasisha vijana na wananchi kuchukua hatua madhubuti dhidi ya uharibifu wa mazingira, pamoja na kueleza umuhimu wa kuboresha na kurejesha mifumo ya ikolojia.
Kwa uteuzi huu, Frida Amani anaingia katika historia kama msanii wa kwanza kutoka Tanzania kushika jukumu hilo, hatua inayotazamwa kama ishara ya kuongezeka kwa nafasi ya wasanii katika kujenga mustakabali endelevu wa mazingira.