Tech news

Watumiaji wa Snapchat Wapata Changamoto Kubwa Kutuma Video na Picha

Watumiaji wa Snapchat Wapata Changamoto Kubwa Kutuma Video na Picha

Kampuni mbalimbali za teknolojia zimekumbwa na changamoto kubwa leo, baada ya huduma za seva zinazotolewa na Amazon Web Services (AWS) kukumbwa na hitilafu ya ghafla ambayo hadi sasa bado haijatatuliwa kikamilifu.

Athari kubwa ya tatizo hilo imeonekana katika matumizi ya programu mbalimbali zinazotegemea AWS kama msingi wa uendeshaji wake. Miongoni mwa zilizoathirika pakubwa ni Snapchat, mtandao wa kijamii unaotumika sana na vijana duniani kote.

Kwa mujibu wa ripoti kutoka kwa watumiaji, Snapchat imekuwa haifanyi kazi kikamilifu tangu asubuhi ya leo. Watumiaji wameshindwa kuweka picha au video mpya kutoka kwenye simu zao, huku huduma za mazungumzo (chats) pia zikiripotiwa kuwa na matatizo ya kiufundi. Hata hivyo, machapisho yaliyohifadhiwa tayari kwenye cloud ya Snapchat yanaweza kuonekana, jambo linaloashiria kuwa tatizo kuu lipo katika uwezo wa mawasiliano kati ya app na seva kuu.

Tovuti ya DownDetector, ambayo hufuatilia hali ya upatikanaji wa huduma mtandaoni, imethibitisha ongezeko kubwa la malalamiko kuhusiana na programu hiyo, na pia programu nyingine zinazotumia AWS ikiwemo baadhi ya huduma za benki, e-commerce, na michezo ya mtandaoni.

Hadi kufikia sasa, kampuni ya Amazon haijatoa taarifa rasmi kuhusu chanzo kamili cha hitilafu hiyo, lakini mafundi wake wanaripotiwa kuendelea na juhudi za kurejesha huduma katika hali ya kawaida.

Amazon Web Services ni mojawapo ya watoa huduma wakubwa zaidi wa seva duniani, na hitilafu yoyote katika mifumo yake huathiri mamilioni ya watumiaji kwa kiwango kikubwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *